NENO LA LEO - JE SILAHA ZAKO ZINA UWEZO?
Tafakari: 2Wakorintho 10:3-5
"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya
mwili; maana Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina UWEZO KATIKA
MUNGU hata kuangusha Ngome; tukiangusha Mawazo na kila kitu
kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila
FIKIRA ipate KUMTII Kristo".
Nakumbuka usemi wa marehemu Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere, wakati
Raisi wa Uganda Idd Amini alipoivamia Tanzania, Baba wa Taifa alisema
"Nia tunayo, Sababu tunayo na Uwezo wa kumpiga tunao". Ndipo akatoa Amri
ya Kumpiga na Kuivunjilia mbali ngome yake katika nchi yake.
Katika ulimwengu wetu huu uliotekwa na Adui shetani, ni jambo la kawaida
kusikia Watu wanajiita ni Wakristo, wengine wanajiita wacha Mungu,
wengine wameokoka n.k. Wanauwezo mkubwa hata wa kuimba nyimbo za dini
kwa hisia kubwa, lakini jambo la kushangaza, asilimia kubwa unawakuta
bado ni watumwa wa yule Adui.
Mbali na kuonekana watu wema au
wacha Mungu machoni pa watu, ndani ya Mawazo yao au Fikira zao, kumejaa
Visasi, Uadui, Kutosamehe, Husuda, Wivu. Wakati mawazo, maneno na
matendo ya Ngono na Mapenzi yakiendelea kukamata akili za Vijana kwa
Wazee, wakipigwa upofu wasione kuwa ni dhambi; Mungu anazidi kutoa wito
wa Kushinda vita.
Wapendwa Ngome kuu za Shetani ziko katika
MAWAZO au FIKIRA, huko ndiko zinatakiwa zivunjiliwe mbali, hatimaye
mawazo yetu yaunganishwe na Kristo. Hayo yanawezekana tu kwa watu ambao
wameruhusu utawala wa Ufalme wa Mungu kuwa ndani yao, kwa njia ya Roho
mtakatifu.
Ni wakati wa kila mmoja kujipima, kuwa je; ni kweli
amezivaa Silaha zenye Uwezo wa Mungu? Mawazo na Fikira Je zinapatana na
Mungu au zimejaa Uchafu wa yule Adui shetani? Yesu Kristo alikuja kwa
ajili ya kutuokoa kutoka katika mateka ya dhambi, na huu ndio uhuru wa
Kweli.
NAWATAKIA WOTE SIKU NJEMA YENYE BARAKA TELE NA MAFANIKIO KATIKA MWILI NA ROHO.
No comments:
Post a Comment