Chumvi inayowawezesha watu kuishi vizuri katika kundi la aina yoyote ni kupendana na kusaidiana, yaani kuwa marafiki kwani Rafiki ni mtu mnayefahamiana,mnayezoeana na kupendana.
MBINU ZA KUANZISHA AU KUTAFUTA MARAFIKI:
-Ukitaka fulani awe rafiki yako basi chukua muda wa kujifunza habari zake kama vile mambo anayopendelea n.k kisha tafuta nafasi ya kukutana na kuongea naye kila mara fursa ya kufanya hivyo inapojitokeza.
-Ikiwa unataka uzungukwe na marafiki wa kweli wakati wote ni lazima ujitahidi kurekebisha tabia yako ili ivute wenzako na kuwafanya wakuthamini na kukuamini.
-Ili watu wavutwe kwako, inatakiwa uonyeshe tabia ya uchangamfu kiasi, usawa, ukweli na nia ya kunufaisha wengine.
MARAFIKI WANA FAIDA GANI?
kuna faida nyingi mbalimbali ambazo mtu ataweza kuzipata kutokana na aina za marafiki alio nao. Kwa mfano rafiki aliye mwandani wake atamfaa sana kwa kuchangamkiana,kuendelezana n.k. Rafiki aliye ahi au sahib wake anakuwa kama ni nguzo yake inayomtegemeza na kumwunga mkono katika mambo yake mengi mbalimbali.Rafiki aliye shoga au mwenzi wake ataweza kumwondolea upweke na wakati huo huo kumpatia nafasi nzuri ya mazoezi kuhusu jinsi ya kuishi na wengine katika uhusiano wa karibu sana.Rafiki aliye somo wake ataweza kumpa ushauri kuhusu mambo mbalimbali yenye manufaa; na rafiki muhimu,ambaye kwa kawaida huwa ni mchumba au mme/mke huongeza furaha na kusaidia katika kutayarisha mambo mbalimbali yaliyo msingi wa maisha ya baadaye.Marafiki wengine wote wa kawaida wenye tabia njema na upeo wa mambo mbalimbali ya kimaisha katika nyanja za kiroho,kiakili na kimwili watasaidia maendeleo na ustawi wetu katika nyanja hizo walizobobea.
RAFIKI WA KWELI NI YUPI?
Rafiki wa kweli ni yule mwenye upendo wa kweli unaojidhihirisha katika kukutakia mema na katika kujali maslahi yako. Kwa kawaida rafiki kama huyo hakuongopei wala hana sura ya kinyonga-yaani hajipendekezi kwako wakati mkiwa pamoja na kukusengenya unapotupa kisogo. Yu mwaminifu kwako katika kila hali. Sio rahisi kupambanua marafiki wa kweli na wala sio rahisi kuwapata wengi wa aina hii.
Ni matumaini yangu kwamba baada ya kusoma maelezo haya mafupi kuhusu marafiki, utaanza kupata nuru mpya ya kuwatazama rafiki zako .
Kwa kukariri ningependa usiache kuzingatia yafuatayo:-
- Jipatie marafiki -wavulana/wanaume kwa wasichana/wanawake.
- Wachague vizuri marafiki hao kutokana na tabia zao njema na manufaa yao kwako.
- Wewe mwenyewe jitahidi uwe mwenye tabia njema, mwenye manufaa kwa rafiki zako, na mwaminifu kwa kila mmoja wao, kadri ya uwezo wako wote.
- Jitahidi kuwafanya watu wenye tabia zisizokubalika katika jamii kuwa marafiki zako kwa kuwabadilisha tabia zao kwa hekima na upole kama Yesu alivyofanya wakati wa maisha yake hapa duniani.Yesu aliwabadilisha watoza ushuru wezi kama Zakayo,makahaba kama Mwamamke msamaria n.k kuwa marafiki wake.
No comments:
Post a Comment