Kanisa(waumini wanaokiri Imani ya Petro kwa Yesu) wamepewa funguo za ufalme wa mbinguni.
angalia nami mathayo 16:19: “Nami nitakupa wewe funguo za
ufalme wa mbinguni”. Kwa maneno mengine Yesu anasema, "Kefa
nitakupa wewe funguo [wewe kefa ambaye hukutetereka kunikiri mimi kama
Masihi na Mwana wa Mungu]. Wewe ni mshika funguo, mlinzi katika malango ya
ufalme.” Unaweza kufunga na kufungua, kuruhusu na kuzuia, wewe ni mlinzi.
Lakini Kefa au waumini wanaokiri imani ya Kefa ni walinzi wa
namna gani mlangoni pa ufalme?
Kabla hatujaelewa
maana ya ufunguo: unakumbuka maneno ya Yesu kwa walimu wa dini katika Luka
11:52? Yesu alisema, “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa
ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.” Mahali
pengine Yesu anawalaumu Mafarisayo (washika dini) kwa kosa hilo hilo (Math
23:13). Mara zote hizo funguo zinasimama badala ya maarifa na ujuzi waliopewa.
Wana-sheria na Mafarisayo walikuwa na ujuzi wa maandiko ambao ungeweza
kuwanufaisha wao na wengine. Lakini hawakutumia maarifa hayo ipasavyo.
Na kwa Petro na waumini wote, ujuzi na maarifa ya ufalme
umetolewa.
Petro na waumini tumefunuliwa na Baba wa mbinguni kumwona Yesu
kama Masihi na Mwana wa Mungu. Ufunuo huo ni ufunguo langoni mwa ufalme. Injili
ya Yesu yaweza kuwafungulia malango ya ufalme wote wanaoipokea na kuwafungia
malango hayo hayo wanapoikataa. Petro na sisi wakristo tumepewa funguo
nyeti.
Lakini mwenzetu Petro alizitumiaje funguo zake? Historia
takatifu imerekodi kwa ufasaha jinsi mtume Petro alivyotumia maarifa ya kumjua
Yesu masihi, kwa mfano:
· Petro alizitumia
funguo hizo siku ya Pentekoste alipowaonesha wayahudi kuwa Yesu ni Masihi
na Mwana wa Mungu aliye hai. Akawaambia, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina
lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi” (Mdo 2:38). Na siku ile wengi kwa
kumsikia Petro na kukubali ujumbe wake walifunguliwa malango ya
ufalme—tunaambiwa maelfu.
· Mara nyingine Petro
alimfungulia malango ya ufalme Kornelio na nyumba yake na wote wakaingia (Mdo
10)
· Mara nyingine
Petro akiwa na Yohana alimfungulia kiwete langoni mwa hekalu naye
akapokea uponyaji
· Mara nyingine Petro na
Yohana wakawafungulia wasamaria nao wakapokea Roho Mtakatifu
·Lakini mara nyingine
Petro alimfungia Anania na Safira na hawakuingia katika ufalme
Funguo alizopewa Petro ndizo tulizopewa. Tumepewa kuwafungulia
watu wamjue Yesu kama Mkombozi nao wafunguliwe. Na kama kila mmoja wetu
aliyepewa funguo hizi atazitumia wangapi wangepokea msamaha wa dhambi, wangapi
wangefunguliwa na utumwa wa dhambi, wangapi wangepokea uponyaji. Yesu
analitambulisha Kanisa kama walinzi katika malango ya ufalme. Ni bahati kuu
kiasi gani lakini ni wajibu mzito namna gani kumiliki funguo za lango kuu la
uzima?
No comments:
Post a Comment