Kabla Yesu hajawaambia wanafunzi wake mtazamo wake juu ya kanisa
alijaribu kuwauliza wao wanamtazamaje. “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa
nani?” (Mathayo 16:13).
Na Yesu akapewa majibu. Majibu tofauti-tofauti kutoka mitazamo
yao tofauti-tofauti. Kulikuwa na hao waliosema Yesu ni Yohana Mbatizaji;
wengine walisema Yesu ni Eliya; Yesu ni Yeremia; Yesu ni mmojawapo wa manabii.
Bila shaka Yesu alihuzunishwa na majibu yao. Kwa sababu Yesu alikuwa zaidi ya
Yohana Mbatizaji, Eliya, Yeremia, au nabii.
Baadaye, Petro akamtuliza Yesu kwa jibu sahii: “Wewe ndiwe
Kristo (Masihi-Mkombozi aliyetumwa na Mungu), Mwana wa Mungu aliye hai?”
Haleluya! Hapo, hapo Yesu akampongeza akimwambia, una bahati, huo sio mtazamo
wa kibinadamu, “mwili na damu havikufunulia hili, bali baba yangu aliye
mbinguni”(fungu la 18). Kwa lugha nyingine, Petro kwa kuwa unanitazama kwa
macho ya imani kama mwana wa Mungu na mkombozi, subiri nitakueleza watu wenye
imani kama yako ninavyowatazama. Kaa chini basi nilitambulishe kanisa langu
kwako kama ninavyolitazama. Yesu anapompongeza Petro kwa kumtambua; hamwiti Petro, isipokuwa
anamwita Simoni Baryona, hilo ndilo jina lake alilopewa na wazazi wake. Petro
ni jina la kupewa-“jina la ubatizo” (Yoh 1:42). Petro lina maana katika
kiyunani kama mwamba. Na katika kiaramaki (lugha mama ya Yesu na Petro) mwamba
huitwa kefa. Kwa kuwa Yesu alikuwa anaongea na Petro kwa kiaramaki bila shaka
Yesu aliongea hivi: “Wewe ndiwe Kefa (mwamba) na juu ya kefa
(mwamba) nitalijenga kanisa langu”
Ni kweli Simoni mwana wa Yona ni sawa na wanadamu wengine.
Lakini hapa Simon ameonesha ukefa, upetro, umwamba. Na ninyi ni mashahidi,
wengi wamechagua kuyumbishwa na upepo wa maoni ya watu kunihusu mimi. Wengi
wameniona kama Yohana Mbatizaji, Eliya, Yeremia, na kama nabii tuu. Lakini hapa
Simon amejibu kama Petro (jiwe); amekataa kusogezwa na maoni ya wengi, kama
mwamba usivyosukumwa na upepo. Petro ni muumini wa kwanza kunikiri mimi kama
Mwana wa Mungu. Imani ya Petro kwangu kama Masihi na Mwana wa Mungu ni
mwamba imara na salama ambao juu yake nitalijenga kanisa langu.
·Katika mathayo 16:16
Petro ni wa kwanza kumkiri Yesu kama Mwana wa Mungu.
·Katika Matendo sura ya
2 Petro ndio wa kwanza kumtangaza Yesu kama Masihi na Mwana wa Mungu kwa
Wayahudi
·Na katika Matendo sura
ya 10 tunamkuta Petro tena kama mhubri wa kwanza wa Yesu kama Masihi na Mwana
wa Mungu kwa Wamataifa.
Kwa kifupi wayahudi kwa wamataifa wanaikiri imaini ile ile ya
Petro kwa Yesu. Kama Petro wakristo leo:
·Tunaamini Yesu ni
Masihi na Mwana wa Mungu hata kama wengine hawaamini hivyo.
·Leo hii tunaamini Yesu
ni Masihi aliyetumwa na Mungu kutukomboa hata kama wengine hawamuoni
hivyo.
·Tunamwona Yesu kama
Mungu mwenye nguvu hata kama wengine wanamwona ni mwana wa Mariam tu.
Na ni imani hii ndio inayotufanya tusalie salama kama jengo
lililosimama mwambani. Imani hii na mtazamo huu ndio mwamba. Msingi wa maoni ya
wengi kuhusu Yesu kama nabii tu, mwalimu tu hautufai kusimamisha imani yetu juu
yake. Misingi hiyo haitulii kama mchanga wa mwambao. Leo ipo kesho imechukuliwa
na maji. Tunaposongwa na mitazamo tofauti tofauti juu ya Yesu ni muhimu
kutoyumbishwa kama Petro. Na tukisimamia katika imani ya Petro tuko salama.
Hivyo, mbele ya macho ya Yesu kanisa la Mungu ni Jengo
linalosimama juu ya mwamba wa imani. Ndivyo linavyosimama mbele ya macho ya
Yesu.
ENDELEA KUJIFUNZA MTAZAMO WA YESU KWA KUNDILAKE DUNIANI. ROHO WA BWANA AWE PAMOJA NAWE.AMINA
No comments:
Post a Comment