Sunday, June 22, 2014

YESU ANAVYOLITAZAMA KANISA LAKE-sehemu ya tatu

Kanisa ni kama Jeshi lililoko uwanja wa vita
Math 16:18. Yesu anasema, “milango ya kuzimu haitalishinda [kanisa langu]” Kwa maneno hayo Yesu analiona kanisa kama Jeshi lililoko vitani linapambana. 

Lakini kanisa linashindana na nani? Linashindana na milango ya kuzimu. Na hapa kuzimu haiwakilishi kitu kingine isipokuwa mauti na kifo (uf 1:18). Kutoka kwa dhambi ya Adamu na wengine tunajua dhambi huzaa mauti (Yak 1:15). Na kama dhambi huzaa mauti, basi kanisa linapambana na dhambi na mauti--baba na mtoto. Adui wa kanisa sio wewe sio mimi na wala si wao; adui wa kanisa sio waislamu wala wapagani, adui wa kanisa sio viongozi wake wala washiriki wake; adui wa mtu sio baba yake, sio mme wake na wala sio watoto wake; labda tu kama wamegeuka kuwa mawakala wa kifo na mauti.

Kanisa halijatulia na haliwezi kutulia, mpaka limeondolewa uwanjani mwa vita, na dhambi na kifo vimetupwa Jehanamu. Wale wanaolilia utulivu na amani watusubiri malangoni mwa Yerusalemu. Huko ndiko hakuna maombolezo wala kilio wala maumivu (ufu 21:4). Wale wanalalamikia magugu yamezidi kutubanaa, uovu umetusonga zaidi, watusubirie siku ya hukumu ambapo wema na wabaya watatenganishwa milele. Kanisa ni Jeshi lililoko vitani, hivyo ndivyo Yesu anavyoliona.

Wewe na mimi tuko vitani. Inawezekana tumemkimbia Yesu, tumemkana hadharani,…. Hilo halitukatishi tamaa, tunajua tuko vitani. Tunaweza kutetereka na kujeruhiwa. Si neno, lakini hatutaitupilia mbali imani yetu. Mapambano yanaweza kuwa makali na majeraha yetu yakatupunguzia damu nyingi na kutuliza usiku kucha, lakini hatutatupilia mbali silaha yetu na imani yetu. Vidole vya wanao tushtumu na kutushtaki vinaweza kuelekezwa mioyoni mwetu na kutukumbusha tulivyomkana Yesu, hatutakata tamaa kutumaini wema wa Yesu. Kama tutabakia uwanja wa vita, hakika tutashinda. Maana Yesu anasema, “milango ya kuzimu”hayatamshinda muumini anayemtumainia Yesu kama Petro. Kama jiwe lililowekwa mlangoni mwa kaburi la Yesu halikuweza kumzuia Yesu siku ya Jumapili ile, kadhalika hata sisi “milango ya kuzimu haitatushinda” tunaposhikilia imani yetu. 

Kujua kuwa kanisa liko vitani kunanifanya nisilikatie tamaa ninapolitazama. Hata mimi kujua niko vitani kunanifanya nisijikatie tamaa katika mapambano ya maisha na imani. Kanisa ni la wapiganaji.


Mbele ya Yesu Kanisa ni zaidi ya jengo lilosimama mwambani, isipokuwa ni  Jeshi linaloshindana vitani. Hivyo ndivyo Yesu anataka kila mmoja alitambue kanisa lake hivyo. Na zaidi ya hapo Yesu analitambua kanisa kama mlinzi wa malango ya ufalme wa mbinguni

No comments:

Post a Comment