Friday, May 23, 2014

ASOMAYE NA AFAHAMU

(ASOMAYE NA AFAHAMU) Mathayo 24:15

Kitabu cha Danieli kinahusu nyakati zetu hizi za mwisho.
Kuelewa mambo yaliyo mbele yetu ni muhimu sana, maana ama
tutapata uzima wa milele, ama mauti ya milele katika mkabala
wetu na matukio hayo yanayokuja. Hivyo si suala dogo kujifunza
unabii wa kitabu cha Danieli kwa wote wanaotaka uzima wa milele.
Yesu akizungumza na wanafunzi wake juu ya matukio ya siku za
mwisho alisema, "Basi hapo mtakapoliona Chukizo la Uharibifu,
lile lililonenwa na Danieli, limesimama mahali patakatifu
(asomaye na afahamu)". Mathayo 24:15. Hatari kubwa i mbele
yetu! Yesu anataka kila asomaye alifahamu Chukizo hilo la
Uharibifu linalokuja ili atakapoliona akimbie kuokoa maisha yake
(Mt. 24:16-22). Chukizo la Uharibifu limetajwa mahali patatu
katika kitabu cha Danieli (Dan. 9:26,27; 11:31; 12:11). Lina
majina mengi katika kitabu cha Danieli na cha Ufunuo ----- Pembe
Ndogo, Mnyama, na kadhalika. Utashangaa kujua kwamba "mnyama"
katika lugha ya taaluma ya unabii sio tusi wala kashfa kama
wengi wanavyodhani. Maana yake ni "mfalme au ufalme"
(Dan.7:17). Biblia inajitafsiri yenyewe!
Hivi maana ya "chukizo" ni nini? Soma 2 Wafalme 21:1-11 na
Kumbukumbu la Torati 18:9-14. Kumbe! Chukizo ni kuabudu
sanamu, kuwaomba wafu, kushughulika na mapepo, uchawi au
ushirikina, kuabudu jua na nyota za mbinguni, na kadhalika.
Mataifa, yaani, wapagani hufanya mambo hayo. Je! "uharibifu"
ni nini? Sio kuharibu vitu, bali ni kuwaangamiza, yaani, kuwaua
watu (Dan.8:24,25). Kwa hiyo, Chukizo la Uharibifu ni mamlaka
au utawala au ufalme unaoabudu sanamu, unaowaomba wafu, ulio na
ushirikina, na, zaidi ya hayo, unaowaangamiza "watakatifu",
yaani, "hao wazishikao Amri [Kumi] za Mungu na Imani ya Yesu
(Ufu.14:12; Kut. 20:3-17; Yak. 2:10-12). Paulo analiita "mtu
wa kuasi, mwana wa uharibifu [mwuaji], mpingamizi [au Mpinga
Kristo] (2 The. 2:3,4].
Bila kila mtu kumjua huyo, Yesu Kristo hawezi kuja duniani.
Tutaendelea kusumbuka na magonjwa, umaskini, na dhiki. Je! si
jambo la muhimu kabisa kuijua mamlaka hiyo ili kujua la kufanya
kuokoa maisha yetu, si yale ya kimwili, bali ya kiroho ili
tupate kuishi milele? (Mt. 10:26-33; Yoh.6:39-40; Ufu.12:11).
Kufa au kutokufa si hoja, bali kujiweka tayari kumlaki Yesu
Kristo atakapokuja juu ya mawingu ya mbinguni (Ufu. 2:10; Mt.
24:29-31).
Mpendwa Msomaji, je! kwa neema yake Mungu unataka kuwa
tayari kujiunga na watakatifu ulimwenguni kote? Soma Danieli,
na ufahamu. Kabla hujaanza kusoma somo, omba ili Mungu akupe
Roho wake atakayekufundisha kweli yote (Yohana 16:13-15). Mungu
na akubariki!

ENDELEA KUTEMBELEA BLOG HII KILA SIKU UJUE MANENO YA UNABII

No comments:

Post a Comment