"MJIFUNZE KWANGU"
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Mathayo 11:29.
"Mjifunze kwangu," alisema yule Mwalimu wa Mbinguni, "kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo...." Yatupasa kujifunza kujikana nafsi, yatupasa kujifunza ujasiri, saburi, ushupavu, na upendo unaosamehe.... Iwapo tunayo imani ndani ya Yesu kama msaidizi wetu, iwapo macho yetu ya imani
yanaelekezwa kwake kila wakati, basi,tutakuwa kama Yesu katika tabia zetu. Atakaa ndani ya mioyo yetu, nasi tutakaa ndani yake Kristo. Tukiwa tumevikwa haki ya Kristo, maisha yetu yanafichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Atakuwa mshauri wetu. Tukimwomba kwa imani, atatufungua ufahamu wetu.... Mafundisho aliyotupa Kristo yatawekwa katika matendo.
Kristo, Kielelezo Chetu, anapowekwa daima mbele ya macho ya akili zetu, hapo ndipo tabia mpya zitaweza kukuzwa, mielekeo yetu mibaya yenye nguvu tuliyorithi pamoja na ile tuliyojizoeza wenyewe itaweza kudhibitiwa na kushindwa, kujisifu kwetu kutatupwa mavumbini, tabia mbaya za zamani za mawazo zitapingwa daima, kupenda kwetu makuu
kutajionyesha katika tabia yetu kwa dhahiri na kudharauliwa, nasi tutakushinda.
Kristo hana budi kuingia katika mawazo yetu yote, hisia zetu zote, na mapenzi yetu yote.
Anapaswa kutukuzwa katika mambo madogo sana ya utumishi wetu wa kila siku katika kazi ile aliyotupa kufanya. Wakati tunapoketi miguuni pake Yesu, badala ya kutegemea
ufahamu wetu wa kibinadamu au kufuata maneno ya hekima ya ulimwengu huu,tunapaswa kuyapokea maneno yake kwa shauku, tukijifunza kwake, na kusema, "Bwana,wataka mimi nifanye nini?" hapo ndipo hali yetu ya asili ya kujitegemea wenyewe, yaani,
kujitumainia wenyewe, kufuata mapenzi yetu wenyewe, itabadilika, na mahali pake itakuwapo roho ile ya kitoto, tiifu, inayokubali kufundishwa. Tunapokuwa na uhusiano sahihi na Mungu wetu, tutaitambua mamlaka ya Yesu katika kutuongoza sisi, na madai
yake kwetu kwamba tumpe utii usiokuwa na maswali.
Tutakuwa na mawazo ya hali ya juu kumhusu Yesu Kristo hata nafsi zetu zitajishusha chini. Mapenzi yetu yatakuwa ndani ya Yesu, mawazo yetu yatavutwa kwa nguvu kuelekea mbinguni. Kristo atakuwa hana budi kuzidi, wakati MIMI NINAPUNGUA....
Tutajizoeza kuwa na wema ule ulio ndani yake Kristo, ili sisi tupate kuakisi kwa wengine mfano wa tabia yake.
KUJITIA NIRA YA KRISTO
Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi. Mathayo 11:30.
Kujitia nira ya Kristo, maana yake kufanya kazi kulingana na njia zake, kuwa mshirika mwenzi pamoja naye katika mateso yake na taabu zake kwa ajili ya wanadamu waliopotea.
Katika kuikubali nira yake Kristo ile ya kujizuia na utii, utaiona kwamba imekuwa msaada mkubwa sana kwako. Kujitia nira hii kunakuweka wewe karibu na ubavu wake
Kristo, naye anachukua sehemu ile iliyo nzito kuliko zote ya mzigo huo.
Nira na msalaba ni nembo zinazowakilisha jambo lile lile moja ----- kusalimisha mapenzi [nia] yetu yote kwa Mungu. Kujitia nira kunamwunganisha mwanadamu katika urafiki pamoja na yule mpendwa sana Mwana wa Mungu. Kuuinua msalaba juu
kunaiondoa nafsi moyoni, na kumweka mwanadamu mahali ambapo anajifunza kubeba mizigo yake Kristo. Hatuwezi kumfuata Kristo bila kujitia nira yake, yaani, bila kuuinua juu msalaba wetu, na kujitwika na kumfuata. Kama mapenzi yetu hayapatani na matakwa yale ya mbinguni, basi, inatupasa sisi kuyakataa matakwa yetu, kuachana na tamaa zetu tunazozipenda sana, na kukanyaga katika nyayo zake Kristo....
Wanadamu hujitengenezea nira ambazo huonekana kuwa ni nyepesi na za kupendeza kuvaa kwa ajili ya shingo zao wenyewe, lakini matokeo yake ni kwamba zinachubua vibaya mno. Kristo analiona jambo hilo, na kusema, "Jitie nira yangu. Nira ile unayoweza kuitia shingoni mwako, ukidhani inakufaa sana, haitakufaa hata kidogo. Jitie nira yangu, nawe ujifunze kwangu mafundisho ambayo ni ya muhimu kwako kujifunza."
Kazi yako sio kukusanya mizigo yako mwenyewe.... Mara nyingi sisi tunafikiri kwamba tuna wakati mgumu katika kuibeba mizigo yetu, na mara nyingi mno mambo yanakuwa hivyo, kwa sababu Mungu hajaweka mpango wo wote kwa ajili yetu kuibeba mizigo
hiyo; lakini tunapojitia nira yake na kuibeba mizigo yake, hapo ndipo tunaweza kushuhudia kwamba nira ya Kristo ni laini na mizigo yake ni myepesi, kwa sababu yeye ameweka mpango wa kuibeba hiyo [mizigo yake].
Hata hivyo, nira hiyo haitatupatia sisi maisha ya raha na uhuru na kujifurahisha nafsi zetu. Maisha yake Kristo yalikuwa ni maisha ya kujitoa mhanga na kujikana nafsi kwa kila hatua [aliyokwenda]; na kwa upendo unaodumu daima kama ule wa Kristo, mfuasi
wake wa kweli atatembea katika nyayo za Bwana wake; naye atakapokuwa anasonga mbele katika maisha haya, atazidi kujazwa na roho ile ile na maisha yale yale ya Kristo.
TUKIJIKANA NAFSI,NAFSI ZETU ZITAKUFA NA NAFSI YA KRISTO ITAISHI NDANI YETU.
No comments:
Post a Comment