Saturday, May 31, 2014

UJUE MOYO WAKO-sehemu ya tatu

NGUVU HALISI YA NIA 
Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo. 2 Wakorintho 8:12.
Dini iliyo safi inahusika na matumizi ya nia. Nia ni uwezo unaotawala katika maumbile
ya mwanadamu, ikiuleta uwezo mwingine wote uliomo mwilini chini ya mamlaka yake.
Nia si kuonja wala mwelekeo, bali ni uwezo wa kuamua la kufanya ambao unafanya kazi
yake ndani ya wana wa wanadamu ama ukiwaelekeza kwenye utii kwa Mungu, ama kwenye uasi....
Bila shaka wewe unatamani kuyafanya maisha yako kuwa kama vile ambavyo yangefaa kukuwezesha kuingia mbinguni hatimaye. Mara nyingi unakata tamaa unapojiona mwenyewe kuwa u dhaifu katika uwezo wako wa kimaadili [tabia], unajikuta u mtumwa wa mashaka, tena umetawaliwa na tabia na desturi za maisha yako ya zamani ya dhambi.... Ahadi zako [maazimio yako] ni kama kamba zilizotengenezwa kwa mchanga....
Daima utakuwa hatarini mpaka hapo utakapoielewa nguvu halisi ya nia yako. Unaweza kuamini na kuahidi mambo yote, lakini ahadi zako au imani yako haina maana yo yote
mpaka hapo utakapoiweka nia yako nyuma ya imani yako na nyuma ya matendo yako.
Kama wewe unapiga vita ile ya imani kwa uwezo wako wote wa nia yako, utashinda.
Hisia zako, mvuto wako, mapenzi yako ya moyoni, mambo yote hayo hayaaminiki, kwa sababu hayawezi kutegemewa....
Lakini wewe huna haja ya kukata tamaa.... Ni juu yako mwenyewe kuisalimisha nia yako kwa nia ile ya Yesu Kristo; nawe unapofanya hivyo, Mungu atakushika mara moja na kufanya kazi yake ndani yako ili upate kutaka na kutenda yale yampendezayo Yeye.
Mwili wako wote ndipo utakuwa chini ya utawala wa Roho wake Kristo, na hata mawazo yako yatatawaliwa naye. Huwezi kuzitawala hisia zako, wala mapenzi yako ya moyoni, kama unavyotaka mwenyewe; lakini unaweza kuitawala nia yako [maamuzi yako], nawe kwa njia hiyo unaweza kufanya mabadiliko kamili katika maisha yako. Kwa kuisalimisha nia [mapenzi] yako kwa Yesu, maisha yako yatafichwa pamoja na Kristo katika Mungu na kuunganishwa na mamlaka ile ipitayo falme zote na mamlaka zote.
Utakuwa katika nguvu yake; na nuru mpya, yaani, nuru ile ya imani iliyo hai, itawezekana kwako kuwa nayo. Lakini nia yako ni lazima ishirikiane na nia yake Mungu....
Je! wewe hutasema, "Nitampa Yesu nia yangu, nami nitafanya hivyo sasa hivi," na kuanzia dakika hii hutakuwa upande wake Bwana kabisa? 

No comments:

Post a Comment