Thursday, May 29, 2014

UJUE MOYO WAKO-sehemu ya pili

KUJIANDAA KWA SHULE ILE YA JUU ZAIDI

Uniongoze katika kweli yako, Na kunifundisha. Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu
wangu, Nakungoja Wewe mchana kutwa. Zaburi 25:5.
Wale ambao ni wana wa Mungu hapa duniani wanaketi pamoja na Yesu katika Shule ya
Maandalizi, wakijitayarisha kupokewa katika Shule ile ya Juu Zaidi. Siku kwa siku
tunatakiwa kila mmoja kufanya maandalizi yake mwenyewe; maana katika majumba yale
ya kifalme kule juu hakuna ye yote atakayewakilishwa na mtu mwingine. Kila mmoja
wetu anapaswa kuusikia yeye mwenyewe mwito ule usemao, "Njoni kwangu,... nami
nitawapumzisha...."
Bwana Yesu amekulipia ada ya mafundisho. Yote yakupasayo kufanya ni kujifunza
kwake.
 Upole kama ule wa Kristo utakaoonyeshwa kwa matendo katika Shule ile ya Juu
unatakiwa kuwekwa katika matendo na wakristo wote, wazee kwa vijana, katika Shule
hii ya Chini. Wale wote wanaojifunza katika shule hii ya Kristo wako chini ya mafunzo
wakiongozwa na wajumbe wale wa mbinguni [malaika]; wala haiwapasi kamwe kusahau
ya kwamba wao ni tamasha kwa ulimwengu huu, kwa malaika, na kwa wanadamu.
Wanapaswa kumwakilisha Kristo. Wanatakiwa kusaidiana wenyewe ili waweze kufaa
kuingia katika Shule ile ya Juu zaidi. Wanapaswa kusaidiana kila mmoja na mwenzake ili
wapate kuwa watakatifu na wenye utukufu, na kulizingatia sana wazo lile la kweli
linaloonyesha maana ya kuwa mtoto wa Mungu. Wanapaswa kusema maneno ya kutia
moyo. Wanapaswa kuiinua juu mikono iliyo dhaifu na kuyafanya imara magoti
yaliyolegea. Juu ya kila moyo panatakiwa kuandikwa maneno haya, kana kwamba ni kwa
kalamu yenye ncha ya almasi, "Hakuna kitu cho chote ninachokiogopa, isipokuwa tu
kwamba mimi sitaujua wajibu wangu, au nitashindwa kuutekeleza."...
Moyo uliodhibitiwa, maneno ya upendo na upole, humletea heshima Mwokozi wetu.
Wale wasemao maneno ya upole, maneno ya upendo, maneno yaletayo amani,
watatunukiwa vizuri sana.... Tunapaswa kumruhusu Roho wake kuangaza katika maisha
yetu ya nje ule upole na unyenyekevu wa moyo tuliojifunza kwake.
Yesu ndiye Mwalimu wetu Mkuu.... Anapenda sana, tena yu tayari sana kukuchukua
wewe katika ushirika wa karibu sana na Yeye mwenyewe. Yu tayari kukufundisha jinsi
ya kuomba kwa imani yenye matumaini na uhakika kama ile ya mtoto mdogo.
Jiandikishe upya jina lako kama mwanafunzi wa shule yake. Jifunze kuomba kwa imani.
Pokea maarifa yake Yesu.
Je! wewe huwezi kuketi miguuni pake Yesu na kujifunza kwake?

MUNGU ATUVUTE KWAKE TUJIFUNZE KWAKE KWANI YEYE NI MNYENYEKEVU WA MOYO.


2 comments:

  1. Mungu akubariki na aendelee kukufunulie maandiko mengine ya kutuandikia ili tujifunze.naomba utuandikie mistari mengine apart fro zab25;5 ambayo itatusaidie tujiandikishe upya majina yetu kama wanafunz wa shule yake.naomb uniandikie maana nzuri ya kujiandikisha upya jina

    ReplyDelete
    Replies
    1. kujiandikisha jina upya kama mwanafunzi wa Yesu ni kuweka upya nia ya dhati ya kumfuata Yesu na mafundisho yake kwa moyo wote kama mtoto mdogo afanyavyo katika kupokea mafundisho kutoka kwa mama yake (kuongoka).matendo 3:19-26
      kuibadili tabia yetu ya dhambi na kulifikia kusudi la Mungu kwa kukaa ndani ya Kristo. Yohana 15:5-8
      kujitahidi kumjua Yesu kwa kujifunza neno la Mungu, kuomba kwa Imani na kushuhudia. Zaburi 119:9-11, mathayo 26:41,Ufunuo 12:11,
      Wafilipi 3:13-14.
      Kumtafuta Mungu kwa moyo wote.Yeremia 29:12-13,Ebr. 11:6

      Delete