Thursday, May 29, 2014

UJUE MOYO WAKO...sehemu ya kwanza

KUJIFUNZA KATIKA SHULE YA KRISTO 
Ni nani amchaye BWANA? Atamfundisha katika njia anayoichagua. Zaburi 25:12.

Yesu amefungua shule kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwapa mazoezi wateule wake, nao wanapaswa kuendelea kujifunza daima kuyaweka katika matendo mafundisho yale anayowapa, ili wapate kumjua kabisa.
Wale wanaofikiri kwamba wao ni wema kiasi cha kutosha, wala hawafanyi kazi kwa bidii katika kuikamilisha tabia yao ya Kikristo, wataweka sanamu mioyoni mwao, nao wataendelea kutenda dhambi katika maisha yao mpaka dhambi kwao itaonekana kuwa si
dhambi tena....

Yesu anajitoa nafsi yake kwa kila mtu aliye mgonjwa, kwa kila mtu anayejitahidi kushinda. Roho Mtakatifu anamwombea kila mpiga mweleka mwaminifu, naye Kristo atayafanya maneno yake kuwa roho na uzima, yaani, kuwa uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila mtu aaminiye. Lakini wewe utashindwa kabisa utakapomruhusu yule mwovu kuutawala moyo wako, yaani, kuyaongoza mawazo yako.... Mungu hatadhihakiwa; hataukubali moyo uliogawanyika. Yeye anataka tumpe huduma yetu yote
kwa moyo wetu wote. Amelipa fedha ya fidia yetu kwa kujitoa nafsi yake mwenyewe kwa ajili ya kila mwana na binti ya Adamu....
Kristo anayo madai juu ya kila mtu; lakini wengi huchagua maisha ya dhambi. Wengine hawataki kuja kwa Yesu ili awape uzima. Wengine husema, "Naenda, Bwana," kwa
mwaliko wake, lakini hawaendi; hawajisalimishi nafsi zao kabisa ili kukaa ndani ya Yesu peke yake, ambamo ni uzima na amani na furaha isiyoneneka, yenye utukufu.... Je! hatutaamka na kuwa na hekima na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya umilele? tafuteni
neema yake Kristo kwa moyo  wote, kwa uwezo  wote, na kwa nguvu  zote.

Mungu ametupa  haki ya kumshikilia Yeye kwa njia ya maombi ya imani. Maombi yaliyojaa imani ndicho kiini cha dini safi, ni nguvu ya siri aliyo nayo kila Mkristo.
Tafuta muda wa kuomba, kuyachunguza Maandiko, kuiweka nafsi yako chini ya nidhamu ya Yesu Kristo. Uishi kwa kuwasiliana na Kristo aliye hai, na mara tu unapofanya hivyo, atakuchukua na kukushika kwa mkono wake ulio imara ambao hautakuachilia kamwe.

UBARIKIWE UNAPOFANYA MATENGENEZO KWA KUUJUA MOYO WAKO NA NEEMA YA BWANA WETU YESU KRISTO IWE NAWE DAIMA.

2 comments:

  1. Ujumbe mnzuri nifanyaje niwe mwana maombi?

    ReplyDelete
  2. MRUDIE BWANA KWA MOYO WOTE UJITIE NIRA YA KRISTO.
    Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye na haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Isaya 55:7,8.
    Ni mawazo yako yasemayo kwamba makosa yako na maasi yako yamekuwa mengi mno kiasi kwamba Bwana hawezi kuyastahi maombi yako, wala kukubariki na kukuokoa
    wewe.... Kadiri unavyozidi kumkaribia Yesu, ndivyo kadiri utakavyojiona kuwa una
    kasoro nyingi sana; maana kuona kwako kutakuwa safi zaidi, na upungufu wako
    utaonekana kwa mapana yake na kwa dhahiri kuwa uko tofauti na tabia yake takatifu.
    Lakini, basi, usikate tamaa. Huo ni ushahidi kwamba madanganyo ya Shetani
    yamepoteza nguvu yake; kwamba mvuto ule unaohuisha wa Roho wa Mungu unakutia nguvu, na kule kutojali kwako na kutojihusisha na maombi kunatoweka.

    ReplyDelete